Mahakama moja kaskazini-magharibi mwa Urusi imemhukumu raia wa Marekani kifungo cha siku 14 jela baada ya kushtakiwa kwa kutunga 'ujumbe wa Kiukreni' kwenye simu yake, kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari vya eneo la Pskov nchini Urusi.
Alexander Antonov, ambaye pia ana uraia wa Urusi, inadaiwa aliandika maneno "Slava Ukraine" ("Utukufu kwa Ukraine") kwenye simu yake, kulingana na ripoti. Haijulikani wazi ikiwa kifungu hiki kiliandikwa katika muktadha wa faragha au kilionekana hadharani.
Mnamo Januari 2024, Wizara ya Haki ya Urusi iliainisha maneno haya kama 'ishara ya Wanazi' na 'kauli mbiu ya Wanazi'. Chini ya sheria ya Urusi, kuonyeshwa hadharani au utangazaji wa 'alama za Nazi' kunaweza kusababisha kifungo cha hadi siku 15 jela.
Maafisa wa mpaka wa Urusi wamedaiwa kugundua msemo huo walipokuwa wakikagua simu ya Antonov kwenye kivuko cha mpaka kati ya Estonia na mkoa wa Pskov nchini Urusi. Ripoti hiyo haikufafanua ikiwa Antonov alikuwa akiingia au kuondoka Urusi.
Kwa mujibu wa ripoti hizo Mahakama ya Wilaya ya Pechora ilikuwa imeamuru kutwaliwa kwa simu ya Antonov pamoja na kumhukumu kifungo cha siku 14 jela.
Kesi ya utawala ya Antonov haikuweza kupatikana kwenye tovuti ya mahakama, kwa hiyo bado haijulikani wakati mawakala wa mpaka wa Kirusi walikagua simu ya Antonov na muda wa kesi yake.
Kufuatia uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine mnamo Februari, 2022, mamlaka ya Urusi imeweka maelfu ya vifungo vya jela na faini kwa watu binafsi kwa kukosoa waziwazi vita au kuunga mkono Ukraine.